Rais William Ruto wa Kenya ametangaza kundi la kwanza la maafisa 400 wa polisi watakaopelekwa Haiti kupambana na ghasia za magenge.
Katika shughuli hii iliyofanyika mjini Nairobi, rais Ruto alikabidhi bendera ya Kenya kwa maafisa ambao watashiriki katika Operesheni ya Kimataifa ya Kulinda Usalama nchini Haiti. Ujumbe huu uliidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Oktoba 2, 2023 chini ya Azimio 2699.
Kupelekwa kwa maofisa hao wa polisi kulikabiliwa na ucheleweshaji na changamoto kadhaa za kisheria, ikiwemo kutangazwa kuwa ni haramu na Mahakama Kuu ya Kenya. Licha ya vizuizi hivi, kundi hilo linatazamiwa kuondoka kuelekea Haiti siku ya Jumanne. Inspekta Jenerali wa Polisi wa Kenya Japhet Koome amemteua msaidizi mkuu wa polisi Godfrey Otunge kama kamanda mpya wa zaidi ya maafisa 2,500 wa polisi wanaohusika katika operesheni hiyo nchini Haiti.
Wiki iliyopita, Kenya ilifikia makubaliano na serikali ya Haiti juu ya utaratibu wa ushiriki wa wafanyakazi wa usalama, wanaoweza kukabiliwa na upinzani mkali wa magenge yenye silaha ambayo yanadhibiti mji mkuu wa Haiti. Zaidi ya polisi 1,000 wa Kenya wanaungana na timu nyingine za kimataifa nchini Haiti kushughulikia ghasia za magenge.