OCHA yasema Sudan inaendelea kutumbukizwa kwenye vurugu
2024-06-25 09:04:59| CRI

Shirika la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu la Umoja wa Mataifa (OCHA) Jumatatu lilisema Sudan inaendelea kutumbukizwa kwenye vurugu huku msukosuko wa kibinadamu ukizidi kuwa mbaya.

Taarifa mpya iliyotolewa na OCHA ilisema watu laki nane ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto, wanaume, wazee na walemavu wako katika hali ya hatari, chini ya mashambulizi yanayoendelea kufanyika kwenye maeneo yenye watu wengi, na kusababisha majeruhi makubwa na ya muda mrefu kwa raia, pamoja na kuharibu vibaya huduma za kimsingi wanazozitegemea sana.

Taarifa imesema katika miezi mitatu iliyopita, watu 143,000 huenda wamepoteza makazi yao huko Al Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan kutokana na mapambano kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).