Serikali ya Kenya imetangaza kuruhusu Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo (KDF) kusaidia kuleta utulivu nchini humo, katika siku ambayo imeshuhudia maandamano yaliyosababisha vifo, majeruhi, majengo ya Bunge kuvamiwa pamoja na uharibifu mkubwa katika miji mbali mbali nchini.
Tangazo hilo limetolewa kupitia Gazeti Rasmi la Serikali jana jioni, na kusainiwa na Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Aden Duale.
Maandamano ya kupinga kupitishwa kwa Mswada wa Fedha 2024 yamefanyika katika kaunti 34 nchini Kenya ikiwemo Nairobi, Mombasa, Eldoret, Nakuru, Meru, na Embu, na yalishuhudia idadi kubwa ya watu, wengi wao wakiwa vijana.
Hata hivyo mswada huo ulipitishwa na Bunge na kwa sasa unasubiri sahihi ya Rais wa nchi hiyo, William Ruto.