Rais wa Kenya asema maandamano ya mtaani ni ya uhaini, jeshi lasambazwa
2024-06-26 09:12:15| CRI

Rais wa Kenya William Ruto amesema maandamano ya mtaani yaliyofanyika Jumanne nchini humo kuwa ni ya uhaini, akibainisha kuwa serikali yake itatoa jibu haraka hivi karibuni juu ya hali hiyo.

Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Ruto alisema serikali imekusanya rasilimali zake zote ili kuhakikisha hali hiyo haitokei tena "kwa gharama yoyote ile". Aliviagiza vyombo vya usalama kutumia njia zote zinazowezekana kuzuia mambo yanayotishia usalama wa taifa, akiongeza kuwa wapangaji, wafadhili na wachochezi wa maandamano hawataachwa huru.

Kauli ya Ruto inakuja saa chache baada ya zaidi ya waandamanaji watano kuuawa kwa kupigwa risasi na wengine zaidi ya 150 kujeruhiwa huku maandamano yakizuka nchini kote kwa wiki ya pili mfululizo ili kupinga mswada wa fedha wa mwaka 2024 nchini Kenya. Majeruhi wamefikishwa katika hospitali mbalimbali ili kupatiwa matibabu ya dharura.