Hamas yakataa mpango rasmi wa Israel wa baada ya vita kaskazini mwa Gaza
2024-06-26 09:13:54| CRI

Hamas imesema mazungumzo ya Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Israel Tzachi Hanegbi kuhusu "mpango wa siku baada ya vita" kaskazini mwa Gaza hayana njia ya kutekelezwa.

Katika taarifa iliyotumwa Xinhua, Hamas ilisisitiza kwamba majadiliano ya Hanegbi kuhusu hatma ya Gaza baada ya vita na mpango wake vinaonesha msisitizo wa serikali ya Israel juu ya "njia isiyo na maana".

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa mustakabali wa Ukanda wa Gaza unapaswa kuamuliwa na watu wa Palestina pekee, na kuongeza kuwa upinzani wake utakata jaribio lolote la kuingilia kati hatma ya watu wao na mustakabali wake. Hanegbi alisema mpango wa siku baada ya vita kwa ajili ya Hamas umeandaliwa katika wiki za hivi karibuni, na hivi karibuni utatekelezwa kwa vitendo.

Wakati huohuo kundi la Houthi la Yemen Jumanne lilidai kuhusika na shambulio la kombora dhidi ya meli ya "Israeli" katika Bahari Arabu. Akiongea katika taarifa iliyopeperushwa na TV ya al-Masirah inayoendeshwa na Houthi, msemaji wa jeshi la Houthi, Yahya Sarea amesema vikosi vya wanamaji vya Houthi vilifanya operesheni ya hali ya juu ya kijeshi vikilenga meli ya Israeli, MSC SARAH V, katika Bahari Arabu, ambapo shambulio hilo lilikuwa sahihi na la moja kwa moja.