Askari 20 wauawa katika shambulio la kigaidi nchini Niger
2024-06-26 14:13:10| cri

Wizara ya Ulinzi ya Niger imesema, askari 20 wameuawa na wengine 9 kujeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililotokea jana asubuhi kwa saa za huko katika mkoa wa Tillabery ulioko magharibi mwa nchi hiyo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Wizara hiyo imesema kikosi maalum cha askari wa ulinzi na usalama kilishambuliwa na muungano wa makundi ya kigaidi pembezoni mwa kijiji cha Tassia na kusababisha vifo vya askari 20 na raia mmoja na magari mawili ya jeshi pia yaliharibiwa katika shambulio hilo.

Wizara hiyo imesema, magaidi kadhaa waliuawa na vyombo vyao vya usafiri na mawasiliano kuharibiwa, na kuongeza kuwa, vikosi vya ziada vya jeshi la anga na nchi kavu vimepelekwa katika eneo la tukio ili kuwasaka washambuliaji waliotoroka.