Rais wa Kenya aondoa mswada wa fedha huku maandamano yakisababisha ghasia
2024-06-27 09:03:26| CRI

Rais wa Kenya William Ruto Jumatano alitangaza kuwa serikali yake imeondoa mswada mpya wa fedha 2024, ambao ulizua maandamano nchini kote tangu Juni 18 wakati mswada huo ulipotangazwa kwa mara ya kwanza.

Katika mkutano na wanahabari mjini Nairobi, Ruto alisema kuwa serikali itatekeleza hatua za haraka za kubana matumizi, zikiwemo kupunguza bajeti ya usafiri ya rais na ununuzi wa magari. Hatua hizi pia zitatumika kwa kaunti na wizara.

Tangazo hilo limetolewa baada ya maandamano kuleta ghasia jijini Nairobi Jumanne na kusababisha vifo vya watu sita na zaidi ya 150 kujeruhiwa. Waandamanaji waliokuwa wakiimba nyimbo za kuipinga serikali, walivunja eneo la bunge lenye ulinzi mkali na kusababisha uharibifu wa mali na kuchoma moto sehemu ya jengo hilo.

Maandamano hayo yalichochewa na nyongeza ya kodi katika Muswada wa Sheria ya Fedha wa 2024, ambao ulilenga kukusanya nyongeza ya shilingi bilioni 346.7 (kama dola bilioni 2.67 za Kimarekani) ili kufadhili bajeti ya serikali ya dola bilioni 31 kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025. Kufuatia kupitishwa kwa mswada huo bungeni Jumanne, Ruto aliamua kutousaini, kutokana na kilio cha umma dhidi ya mswada huo.