Tanzania yashika nafasi ya 5 duniani kuvutia watalii kimataifa
2024-06-27 11:00:51| cri

Takwimu zilizotolewa na Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) zimeonyesha kuwa, Tanzania imeweka rekodi ya kimataifa kwa miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu kwa kushika nafasi ya 5 kwa nchi iliyovutia watalii zaidi duniani, na nafasi ya kwanza barani Afrika kwa kuvutia watalii kimataifa.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Maliasili na Utalii wa nchi hiyo, Angellah Kairuki katika kikao cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma, alipokuwa akichangia mjadala wa Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025, na Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Amesema pia Tanzania imeshika nafasi ya 4 kwa takwimu za January mpaka Machi, 2024 katika nchi zilizoongeza mapato yanayotokana na shughuli za utalii duniani na kushika nafasi ya kwanza Barani Afrika.