Wamiliki wa maduka nchini Tanzania wagoma kutokana na mrundikano wa kodi
2024-06-27 09:02:17| CRI

Wamiliki wa maduka katika mikoa sita ya Tanzania wamefunga maduka yao kupinga utaratibu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kutoza kodi kwa kutumia mashine ya kielektroniki. Mgomo huo ulianza Jumatatu katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam. Baadaye ulienea katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Dodoma, Mtwara, na Arusha.

Jumatano, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikutana na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara mjini Dodoma, lakini hakuna taarifa rasmi iliyotolewa baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo.

Jumatatu, serikali ilisitisha zoezi la ukaguzi wa risiti za kielektroniki na ritani za kodi uliokuwa ukifanywa na TRA ikisubiri mapitio ya mfumo wa ukusanyaji wa kodi.

Uamuzi wa kusitisha ukaguzi wa risiti za kielektroniki ulifikiwa katika kikao cha mawaziri wa fedha, biashara, na mipango na viongozi wa vyama vya wafanyabiashara na wakala wa udhibiti kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Siku ya Jumatatu, Wabunge waliitaka serikali kutoa majibu thabiti kuhusu mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea, wakisema hali hiyo inahatarisha uchumi wa nchi.