Serikali ya Tanzania yapiga marufuku tozo kinyume na sheria kwa wachimbaji wa madini
2024-06-27 23:00:08| cri

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini imepiga marufuku Halmashauri zote nchini humo kutoza tozo kwa wachimbaji wa madini ambazo hazikubaliana na sheria kuu.

Naibu Waziri wa Madini wa Tanzania, Dk. Steven Kiruswa, amesema hayo jana katika Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA). Dk. Kiruswa amesema tozo yoyote inayotozwa katika sekta ya madini lazima iwekwe kulingana na sheria kuu.

Dk. Kiruswa pia alitangaza kuanzishwa kwa kliniki ya kusikiliza na kutatua changamoto za wadau wa sekta ya madini kuanzia Julai 3, 2024, na kliniki hiyo itafanyika kwa kushirikiana na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde. Amesisitiza kuwa, kupitia kliniki hiyo, changamoto zote zinazoweza kutatuliwa papo hapo zitashughulikiwa, na zile za kisheria na kimfumo zitashughulikiwa kwa kushirikiana na wadau husika.