Wanasayansi watoa wito wa kukomesha uwindaji wa tembo kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania
2024-06-28 08:59:35| CRI

Timu ya wanasayansi wa kimataifa imesema uwindaji wa tembo kwenye mpaka wa Kenya na Tanzania kwa ajili ya meno yao unapaswa kukomeshwa ili kuokoa wanyama hao wakubwa wa nchi kavu wasije kutoweka.

Katika barua iliyochapishwa na jarida la kimataifa la Sayansi, wanabiolojia 24, wataalamu wa wanyama, na wahifadhi walionya dhidi ya uwindaji wa nyara za ndovu kwenye mfumo wa ikolojia wa Amboseli uliopo kwenye eneo la mpaka wa Kenya na Tanzania, kitendo ambacho kinaleta tishio kwa utalii na maisha ya jamii za wenyeji.

Kwa mujibu wa wanasayansi, ndovu watano dume waliokuwa na meno yenye uzito wa karibu kilo 45 walipigwa risasi na wawindaji wa nyara nchini Tanzania mwishoni mwa 2023 na mapema mwa 2024, na hivyo kuleta tishio jipya kwa maisha ya wanyama hao. Tembo hawa, walikuwa miongoni mwa spishi zilizofanyiwa utafiti kwa miaka 51 na Mradi wa Utafiti wa Tembo wa Amboseli (AERP) nchini Kenya.

Licha ya kupigwa marufuku nchini Kenya kwa miaka 50 iliyopita, uwindaji wa nyara unaruhusiwa katika nchi jirani ya Tanzania japo wawindaji hawaruhusiwi kuwapiga risasi karibu na Hifadhi ya Kitaifa ya Amboseli ili kusaidia kulinda wanyama hao wanaovuka mpaka.