Umoja wa Mataifa umeonya juu ya hatari ya baa la njaa katika maeneo 14 kote Sudan.
Ukinukuu ripoti mpya kuhusu Uainishaji wa Awamu ya Usalama wa Chakula Jumuishi inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ambao ni mpango wa washirika mbalimbali wa kuboresha usalama wa chakula na kufanya maamuzi, Umoja wa Mataifa umesema kwenye tovuti yake kwamba hatari ya baa la njaa inatishia wakaazi, watu walioondoka kwasababu ya vita na wakimbizi katika maeneo yasiyopungua 14 yakijumuisha majimbo ya Darfur, Greater Kordofan, na Al Jazira, pamoja na maeneo ya Khartoum.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa watu milioni 8.5, au asilimia 18 ya watu wote wa Sudan, sasa wanakabiliwa na awamu ya nne ngazi ya "dharura" ya uhaba wa chakula. Mbaya zaidi, watu laki 7 na elfu 55 wanakabiliwa na awamu ya tano ya hali ya janga katika majimbo 10.