China yashikilia Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani
2024-07-01 08:42:05| CRI

Huu ni mwaka wa 70 tangu China kutoa Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani. Miaka 70 iliyopita, aliyekuwa Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai alipendekeza kwa mara ya kwanza kanuni tano za “kuheshimiana mamlaka na ukamilifu wa ardhi, kutovamiana, kutoingilia mambo ya ndani, usawa na kunufaishana, na kuishi pamoja kwa amani”. Katika miaka 70 iliyopita, kanuni hizo zimekubaliwa na nchi mbalimbali duniani, na zimekuwa kanuni za kimsingi za kimataifa.

Miaka 70 iliyopita, China ilipendekeza Kununi Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani kutokana na maumivu yake ya kihistoria. Tangu vita vya Afyuni mwaka 1840, China ilianza kupoteza uhuru na usawa, ambapo ilivamiwa na kukandamizwa vibaya na nchi mbalimbali za kibeberu, mpaka Jamhuri ya Watu ya China ilipoanzishwa, na mikataba yote isiyo na usawa kati ya China na nchi za kibeberu kuondolewa.
Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani zinaendana kwa kina na Katiba ya Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa Katiba hiyo, madhumuni na kanuni za Umoja wa Mataifa ni kudumisha amani na usalama wa kimataifa, kuheshimu haki sawa za watu, kuheshimu mamlaka halali za nchi zote, kutatua migogoro ya kimataifa kwa amani na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa.
Kinyume cha Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani ni Umwamba. Nchi zinazofanya umwamba hupuuza usawa katika sera zao za kidiplomasia, zinaamini kwamba nchi yenye nguvu inaweza kufanya chochote, na haina haja ya kujali maslahi ya nchi nyingine. Mwanzoni, mara China ilipotoa Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani, zilikaribishwa na kukubaliwa na takriban nchi 30 za Asia na Afrika ambazo zilikuwa zimepata uhuru kutoka kwa nchi za kikoloni, na kuanza kuwa silaha yenye nguvu ya kiitikadi kwa nchi zinazoendelea kushirikiana na kupambana na vitendo vya kimwamba vya nchi za magharibi.
Katika miaka 70 iliyopita, nguvu ya China imekua kwa haraka, na China imebadilika kuwa nchi kubwa zaidi ya kiviwanda kutoka nchi dhaifu ya kilimo. Lakini hali isiyobadilika ni kwamba China siku zote inashikilia Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani katika sera zake za kidiplomasia. Katika mambo ya kijeshi, China inaheshimu mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya nchi nyingine, na haijawahi kuvamia nchi yoyote. Katika mambo ya kisiasa, China haijawahi kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, na kushirikiana vizuri na nchi nyingine kukabiliana na umwamba. Katika mambo ya kiuchumi, China imeshirikiana vizuri na nchi nyingine ili kupata mafanikio ya pamoja.
Nchi za Afrika na China zina maumivu yanayofanana ya kihistoria, na zote zilivamia na kukandamizwa na nchi za kibeberu. Kanuni Tano za Kuishi Pamoja kwa Amani zinazotetewa na China zinakubaliwa sana na nchi za Afrika.
Uhusiano kati ya China na nchi za Afrika ulioanzishwa kwa kufuata Kanuni hizo una tofauti ya kimsingi na uhusiano kati ya nchi za kibeberu na Afrika. Katika miaka 70 iliyopita, China siku zote imeendeleza uhusiano na Afrika kwa mujibu wa Kanuni hizo, na kupata mafanikio makubwa.