Zambia yatoa wito wa kuimarisha mifumo ya afya ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa ya mlipuko barani Afrika
2024-07-01 08:42:36| CRI

Waziri wa Afya wa Zambia Sylvia Masebo amesema kuongezeka kwa magonjwa ya milipuko hivi karibuni barani Afrika ni kiashiria cha haja ya dharura ya nchi za bara hilo kuboresha mifumo ya afya inayolenga shughuli za uratibu na maandalizi ya mapema ya kujibu majanga hayo.

Akizungumza katika mkutano wa tatu wa Tume ya Uongozi ya Mawaziri wa Kikanda ulioandaliwa na Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) uliofanyika mjini Lusaka, Bi. Sylvia amesema pamoja na kwamba mafanikio yamepatikana katika kupambana na milipuko ya magonjwa na magonjwa ya kuambukiza, matishio mapya yameendelea kutokea, na kuongeza mzigo wa mifumo ya afya. Pia amesema, kuna haja ya kujenga na kuimarisha mifumo ya afya ili kuhakikisha kuwa ni nyumbufu, yenye uwezo na kuziwezesha jamii kustawi.

Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC Jean Kaseya amesema, ni muhimu kwa nchi za Afrika kuzungumza kwa sauti moja katika kukabiliana na milipuko ya magonjwa katika bara hilo. Amesema mwendelezo wa milipuko ya magonjwa inadhoofisha mifumo ya afya ya bara hilo, na hivyo kuwa haja ya ushirikiano zaidi katika sekta hiyo.