ATMIS yakabidhi kambi ya 4 ya jeshi kwa Somalia
2024-07-01 08:41:32| CRI

Tume ya Mpito ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) imekabidhi kambi ya jeshi ya Abdalle Birolle kwa Jeshi la Somalia, ikiashiria kuhamishwa kwa kambi ya nne ya kijeshi kama sehemu ya awamu ya tatu ya kuondoka kwa kikosi cha ATMIS.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, ATMIS imesema kambi hiyo ambayo awali ilikuwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Ulinzi la Kenya katika ATMIS, iko katika mkoa wa Jubaland, kusini mwa Somalia.

Naibu mwakilishi maalum wa Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika nchini Somalia, Sivuyile Thandikhaya Bam aliyekabidhi kambi hiyo, amesisitiza ahadi ya ATMIS kusaidia mpango wa mpito wa Somalia ili kurejesha amani na utulivu katika kanda hiyo.

Tume hiyo ya Umoja wa Afrika imeondoa askari 5,000 kutoka Somalia na kukabidhi zaidi ya kambi 17 za kijeshi kwa Vikosi vya Usalama vya Somalia wakati wa awamu ya kwanza na ya pili ya kupunguza askari wake zilzokamilika mwaka jana.