Wafanyabiashara wa ufuta Tanzania walalamikia mfumo wa TMX
2024-07-01 10:15:30| cri

Wakulima wa ufuta kutoka Wilaya ya Kilwa huko Tanzania wameiomba Serikali kuangalia upya mfumo wa TMX kwa kuwa umekuwa sio rafiki katika biashara ya zao hilo.

Akizungumza baada ya mnada wa ufuta, mkulima kutoka Kijiji cha Njinjo, Abdulkarim Mkanile amesema bei ya ufuta imeshuka kutoka Sh3,640 mnada wa kwanza hadi kufikia Sh3,490 kwenye mnada wa pili.

Amesema mfumo wa TMX hauwanufaishi wakulima kwa sababu unashusha bei kwa haraka.

Mkanile amesema mfumo wa zamani ulikuwa mzuri zaidi kwa sababu mnunuzi hakuwa na uwezo wa kuona bei iliyowekwa na mnunuzi mwenzake.

Mkulima Abdalah Hassan amesema hali ikiendelea hivyo, huenda baadhi ya wakulima wakazuia ufuta wao ndani na kutafuta masoko nje ya ushirika.

Hata hivyo, Ofisa Ushirika wa Mkoa wa Lindi,  Projestus Pascal amewataka wakulima kupeleka ufuta bora ili kuongeza uwezekano wa bei kupanda kwenye minada ijayo.

Jumla ya tani 4,400 zimeuzwa kwenye mnada wa pili wa Chama Kikuu cha Lindi Mwambao, katika AMCOS ya Matandu, Wilaya ya Kilwa kwa bei ya juu ya Sh3,490 huku ya chini ikiwa Sh3,340 kwa kilo moja ya ufuta.