Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bibi Mao Ning amesema China inapinga vikali ripoti ya Kimataifa ya Uhuru wa Kidini ya mwaka 2023 iliyotolewa hivi karibuni na Marekani.
Amesema ripoti hiyo haikutilia maanani mambo halisi, haina ukweli, inazingatia itikadi kali, chuki, na kudharau sera za kidini za China kwa makusudi.
Bibi Mao amesema kuwa, serikali ya China inalinda uhuru wa raia wa kuabudu kwa mujibu wa sheria, na watu wa makabila yote nchini China wanafurahia uhuru kamili wa kuabudu kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu suala la Xinjiang, pia amesema, hivi sasa mkoa huo unafurahia utulivu wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi, umoja wa kikabila, utangamano wa kidini, na kuboresha maisha ya watu.
Amesema Marekani inapaswa kuheshimu ukweli, kurekebisha makosa, na kuacha kutumia masuala ya kidini kuingilia kati mambo ya ndani ya China.