Wazalishaji wa sukari Tanzania wakanusha madai ya kuhodhi sukari huku kukiwa na madai ya mfumuko wa bei
2024-07-02 10:09:59| cri

Chama cha Wazalishaji Sukari Tanzania (TSPA) kimekanusha madai ya kushindwa kuagiza sukari kutoka nje na kuihifadhi sukari ili kupandisha bei kiholela kwa lengo la kujinufaisha.

Chama hicho kimesema wao wakiwa wazalishaji, hawana nia ya kudhoofisha usambazaji wa sukari nchini Tanzania na kwamba wamejitolea kuongeza uzalishaji sukari.

Kauli ya TSPA imekuja kufuatia mjadala wa wabunge waliolalamika vikali kuwa wazalishaji wa sukari wamechangia kupanda kwa bei ya sukari kulikotokea nchini Tanzania mwezi Januari na Februari mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari, mwenyekiti wa TSPA Balozi Ami Mpungwe, amesema walitahadharisha mamlaka mwaka jana kuhusu upungufu wa uzalishaji unaoweza kuathiri usambazaji kuanzia Desemba na kuendelea kutokana na utabiri wa mvua za El Nino.