Watanzania milioni sita wako hatarini kupata upofu
2024-07-02 23:10:57| cri

Watanzania milioni sita wametajwa kuwa hatarini kupata upofu wa kudumu kutokana na kushindwa kupata huduma ya upasuaji wa mtoto wa jicho kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali.

Waziri wa Afya wa Tanzania Bibi Ummy Mwalimu amesema hayo wakati akizundua kituo cha hisani cha matibabu ya macho cha K.S.I mjini Dar es Salaam, na kuongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) watanzania milioni 12 hawana uhakika wa kupata huduma sahihi ya macho hususani katikamaeneo ya vijijini.

Amesema hali hii inaonyesha kuwa bado huduma hazijawafikia watanzania wengi, na watu milioni sita wapo hatarini zaidi kupata upofu. Amesisitiza kuwa juhudi zaidi zinatakiwa katika kufikisha huduma hizo vijijini, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuwahi kupata huduma ya macho ikiwa pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho.