Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umefikia maafikiano ya kihistoria kwa kupitisha azimio linaloongozwa na China kuhusu kuboresha ushirikiano wa kimataifa kwa ujenzi wa uwezo wa akili bandia (AI), huku nchi zaidi ya 140 zikipiga kura ya ndio.
Uamuzi huu wa kihistoria sio tu unaonyesha maafikiano ya kimataifa kuhusu usimamizi wa Akili Bandia, lakini pia unaonyesha nafasi muhimu ya China katika kuongoza uratibu wa kimataifa wa AI.
Akizungumza katika Baraza hilo, mwakilishi wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Balozi Fu Cong amesema, kwa sasa maendeleo ya kasi ya teknolojia ya AI duniani yanakuwa na athari chanya katika maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi zote na maendeleo ya ustaarabu wa binadamu. Amesema hata hivyo kuwa, watu katika nchi nyingi, hususan zinazoendelea, wameshindwa kupata, kutumia, na kunufaika na teknolojia za AI kwa kuwa pengo la kidijitali duniani bado ni kubwa.
Azimio hilo linasisitiza kuwa maendeleo ya AI yanapaswa kushikilia kanuni zinazotanguliwa watu na kunufaisha jamii nzima kwa ujumla.