Serikali ya Tanzania imesema imepokea na itashughulikia malalamiko ya wazalishaji wa mvinyo kuhusu ongezeko la ushuru wa pombe. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) ya Tanzania Prof Kitila Mkumbo, amesema hayo alipotembelea kiwanda cha mvinyo cha Alko Vintages ili kukagua changamoto zinazowakabili wawekezaji wazawa.
Amesema serikali kupitia wizara yake ina jukumu la kutatua changamoto zinazowakabili wenye viwanda vya ndani, na kwamba inawawezesha wenye viwanda hivyo kuchangia pato la taifa, kutengeneza ajira kwa vijana, na kuwapatia wakulima masoko ya mazao.
Profesa Kitila pia ameipongeza kampuni hiyo kuwa na wataalam kutoka Afrika Kusini, nchi inayozalisha mvinyo kwa wingi zaidi barani Afrika, wanaoweza kusaidia kufanya mvinyo wa Tanzania kushindana na ule wa Afrika Kusini.