Rais Xi Jinping wa China jana Jumatano alikutana na rais Sadyr Zhaparov wa Kyrgyzstan huko Astana, Kazakhstan, kabla ya kuhudhuria Mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO).
Rais Xi amesema mwaka jana China na Kyrgyzstan zilitekeleza vizuri makubaliano yaliyofikiwa na viongozi hao wawili mwezi Mei mwaka jana na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili unaendelea kupiga hatua, amesema China inafuraha kuona Kyrgyzstan ni tulivu na inapata maendeleo.
Amesisitiza kuwa nchi hizo mbili zinatarajiwa kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na kuinua kiwango cha mawasiliano. China inapenda kuingiza zaidi bidhaa za mazao ya kijani kutoka Kyrgyzstan na kuhamasisha kampuni za China kuwekeza katika nchi hiyo pamoja na kuimarisha ushirikiano katika sekta za magari ya nishati safi, biashara ya mtandaoni ya kuvuka mipaka n.k. Amesema, China itaendelea kushirikiana na Kyrgyzstan kuimarisha "mfumo wa China na nchi za Asia ya Kati" na kuhakikisha maendeleo ya jumuiya ya SCO katika mwelekeo sahihi kwa maslahi ya pamoja ya pande husika.
Rais Zhaparov amesema Kyrgyzstan itashikilia kithabiti kanuni ya “China Moja” na itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kampuni za China nchini humo. Kyrgyzstan inatarajia kuimarisha mawasiliano na uratibu na China katika mfumo wa pande nyingi ikiwemo SCO.