Rais Xi Jinping wa China tarehe 3 Julai alikutana na mwenzake wa Azerbaijan Ilham Aliyev huko Astana kabla ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO).
Rais Xi amesema China na Azerbaijan ni marafiki wakubwa wa kuaminiana na wenzi wazuri wa kunufaishana. Ziara yake ni mwanzo mpya wa kuinua uhusiano wa nchi mbili hadi kufikia ngazi ya uhusiano wa wenzi wa kimkakati. Amesema Pande zote mbili zinapaswa kuendelea kuungana mkono na kuwanufaisha zaidi watu wa nchi mbili.
Rais Xi amesisitiza kuwa China na Azerbaijan zinapaswa kuhimiza ujenzi wa pamoja wa“Ukanda Mmoja, Njia Moja”, kuimarisha ushirikiano, na kupanua mawasiliano kwenye sekta za elimu, utamaduni, utalii, vijana na jamii.
Rais Aliyev amesema Azerbaijan inapenda kuimarisha ushirikiano na China kwenye sekta za uchumi na biashara, na kudumisha ushirikiano chini ya mifumo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mfumo wa SCO, kupinga uingiliaji kutoka nje, na kulinda usalama na utulivu wa kikanda.