Zaidi ya watu milioni 66 wakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula katika Pembe Kuu ya Afrika
2024-07-04 08:43:34| CRI

Ripoti mpya iliyotolewa jana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Afrika (FAO) na Shirika la Maendeleo la Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD)  imesema, watu milioni 66.7 katika kanda ya Pembe ya Afrika wanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa usalama wa chakula.

Ripoti hiyo imesema, kati ya idadi hiyo ya jumla, watu milioni 39.1 wanatokea nchi sita kati ya nane wanachama wa IGAD, ambazo ni Djibouti, Kenya, Somalia, Sudan Kusini, Sudan na Uganda. Nchi nyingine ambazo watu wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula katika kanda hiyo ni Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ripoti hiyo imezema, mapigano, kupanda kwa gharama za maisha, milipuko ya magonjwa na ukosefu wa lishe bora na maji salama vimeendelea kuathiri usalama wa chakula na lishe katika eneo la Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, matukio mabaya ya hali ya hewa kama mafuriko na ukame, mapigano na milipuko ya magonjwa vinaendelea kusababisha watu kukimbia makazi yao na kufanya mamilioni ya watu kukosa usalama wa chakula.