Bei ya petroli ya rejareja kwa Julai imeshuka katika mikoa inayochukua mafuta hayo bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara ikilinganishwa na Juni, huku dizeli ikiongezeka kidogo.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inaonyesha bei za mafuta imeshuka kwa Sh51 kwa lita na kuwa Sh3,210, huku dizeli ikiongezeka kidogo kwa Sh3 kutoka Sh3,112 hadi Sh3,115 katika mkoa huo.
Hata hivyo, dizeli inayopokewa katika Bandari ya Tanga imeongezeka kutoka Sh3,121 Juni hadi Sh3,124 Julai, pia kwa Bandari ya Mtwara imeongezeka kutoka Sh3,122 hadi Sh3,124 katika kipindi kama hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Mwainyekule kupitia taarifa kwa umma amesema miongoni mwa sababu za kupungua bei ya bidhaa hiyo ni kupungua kwa bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia (FOB).