Kenya kufanyia marekebisho bajeti baada ya kuondolewa kwa muswada wa fedha
2024-07-05 08:44:46| CRI

Rais wa Kenya, William Ruto amesema, serikali yake inafanyia marekebisho bajeti yake baada ya kuondolewa kwa Muswada wa Fedha 2024, ambao umesababisha maandamano makubwa nchini humo katika wiki tatu zilizopita.

Rais Ruto aliyeongoza mkutano wa Baraza la Mawaziri jijini Nairobi hapo jana, amesema Hazina Kuu ya nchi hiyo itapunguza ukubwa wa bajeti ili kuleta uwiano kati ya mambo yanayopaswa kutekelezwa na yanayoweza kusubiri, na kuhakikisha kuwa miradi ya kitaifa haitaathiriwa.

Juni 13, Kenya iliwasilisha bajeti yake ya dola za kimarekani bilioni 30 kwa mwaka wa fedha 2024/2025, iliyolenga kudumisha ukuaji wa uchumi unaotarajiwa kufikia asilimia 5.5 mwaka huu.

Muswada wa Fedha wa mwaka 2024 uliosababisha maandamano nchini humo, ulitaka kuongeza dola za kimarekani bilioni 2.67 kupitia kodi mpya mbalimbali zilizopendekezwa.