Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa yametoa wito kwa nchi za mashariki na kusini mwa Afrika kutunga sheria na sera ili kulinda haki za wasichana wanaopata ujauzito kupata elimu.
Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa jijini Nairobi, Kenya hapo jana, Mkurugenzi mkazi wa UNICEF kanda ya mashariki na kusini mwa Afrika Etleva Kadili na mkurugenzi mkazi wa UNESCO kanda ya Afrika mashariki Alexandros Makarigakis wamesema, inasikitisha kuwa ni nusu tu ya nchi za Afrika zimeweka hatua za kuhakikisha wasichana wanaopata ujauizito wanamaliza shule. Maofisa hao wamesema kuacha shule kwa watoto wa kike kunatokana na mazingira yasiyo salama mashuleni ambayo yamejaa unyanyapaa na kutengwa, na hivyo kuwafanya kuficha ujauzito wao.
Pia wamesema, kati ya wasichana wanaoacha shule kutokana na ujauzito, ni chini ya asilimia 5 wanarejea tena shuleni, ikimaanisha kuwa kupata ujauzito ni ishara ya kumalizika kwa lengo lao la kupata elimu.