Tume ya SADC yakamilisha operesheni dhidi ya ugaidi kaskazini mwa Msumbiji
2024-07-05 08:45:21| CRI

Tume ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SAMIM) imetangaza uamuzi wake wa kuondoa vikosi vyake kutoka mkoa wa Cabo Delgado, kaskazini mwa Msumbiji, na kuashiria kumalizika kwa jukumu lake la ulinzi wa amani katika mkoa huo.

Hafla hiyo iliongozwa na Waziri wa Ulinzi wa Msumbiji Cristovao Chume na Mkuu wa SAMIM Mpho Molomo na ilifanyika katika mji mkuu wa mkoa wa Cabo Delgado, Pemba.

Chume amesema, kambi za magaidi zimeharibiwa na shughuli za kiuchumi zimeanza tena katika mkoa huo, huku watu waliokimbia makazi yao wakirejea na hali ya usalama kuimarika katika mkoa huo.

Ameonya kuwa, licha ya mafanikio na kuondoka kwa vikosi vya SAMIM, bado kuna harakati za kigaidi katika baadhi ya maeneo ya mkoa wa Cabo Delgado, na kusababisha ukosefu wa usalama kwa wakazi wa maeneo hayo.

Tume ya SADC nchini Msumbiji ilipelekwa mwezi Julai, 2021 baada ya kupitishwa na Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi na Serikali za SADC, kama jibu la kanda hiyo kuunga mkono juhudi za Msumbiji katika kupambana na ugaidi.