Wanawake kuweka Uwiano kati ya Kazi na Malezi ya Familia
2024-07-06 09:00:16| CRI

Imezoeleka kuwa nafasi ya mwanamke ni jikoni na kulea familia, na pale mwanamke anapoamua kufanya kazi ama biashara, basi anategemewa kujipanga vizuri ili kufanya kazi zake kwa bidii na pia kulea na kutunza familia. Lakini hali ni tofauti pale inapokuwa upande wa baba, kwani inaonekana kama malezi ya familia na watoto ni ya mama pekee, na baba kazi yake ni kutafuta hela. Inafahamika kuwa kama mtoto akiwa na maadili mabaya lawama moja kwa moja zinakwenda kwa mama, lakini kama akifanya vizuri, utasikia maneno kama ‘ana akili kama baba yake,’ wakati huyo baba anayetajwa wala hajui maendeleo ya mtoto wake!

Malezi ya watoto ni jukumu la wote, baba na mama, na si jukumu la mama peke yake ama baba peke yake. Wote wanapaswa kutenga muda wa kukaa na kuzungumza na watoto wao, wajue maendeleo yao shuleni, changamoto za kimaisha wanazokutana nazo, na kuwashauri kutokana na uzoefu wao, kwa maana kuna msemo kuwa, anachokiona mzee akiwa amekaa, kijana hawezi kukiona hata akipanda juu ya mti wa mkuyu! Basi katika kipindi cha leo cha Ukumbi wa Wanawake tutasikia baadhi ya wanawake wakizungumzia jinsi wanavyoweza kugawa muda wao kutekeleza majukumu yao ya kikazi na pia kutunza familia zao.