Rais wa China akutana na waziri mkuu wa Hungary
2024-07-08 14:59:32| cri

Rais Xi Jinping wa China leo hapa Beijing amekutana na waziri mkuu wa Hungary Viktor Orban, ambaye yuko ziarani nchini China.

Rais Xi amesema China na Hungary zinapaswa kudumisha mawasiliano ya viongozi, kuzidisha hali ya kuaminiana kisiasa, kukuza uratibu na ushirikiano wa kimkakati, kuendelea kuungana mkono, kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali, kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, na kuendelea kuongeza yaliyomo katika uhusiano wao wa wenzi wa kimkakati kwa pande zote na wakati wote, ili kuwanufaisha wananchi wa nchi hizo mbili.

Rais Xi pia ameipongeza Hungary kwa kuwa nchi mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Ulaya, na kusisitiza kuwa uhusiano kati ya China na Umoja wa Ulaya una maana ya kimkakati na kimataifa, unapaswa kuendelezwa vizuri na kwa utulivu, na kukabiliana kwa pamoja na changamoto za kimataifa.

Naye Orban amesema nchi yake inapongeza kazi na ushawishi wa China duniani, na kupenda kuzidisha ushirikiano na uratibu na China. Ameongeza kuwa Hungary inatetea kuimarisha ushirikiano na China, na kupenda kuhimiza maendeleo ya uhusiano kati ya Umoja wa Ulaya na China.