Tanzania imeadhimisha siku ya 3 ya Lugha ya Kiswahili Duniani huku Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Dk. Damas Ndumbaro akitoa wito wa matumizi ya lugha ya Kiswahili katika maeneo mengine muhimu, ikiwa ni pamoja na akili bandia (Al).
Akiongea mjini Dar es salaam kwenye maadhimisho ya siku hiyo, Dk. Ndumbaro amesema Tanzania na dunia kwa ujumla wanatakiwa kufanya ubunifu wa teknolojia za akili bandia na mitandao ya kijamii inayotumia lugha ya Kiswahili, wakati lugha hiyo ikiwa inaenea kwa kasi kubwa.
Dk. Ndumbaro pia ameliagiza Baraza la Taifa la Kiswahili na Baraza la Kiswahili la Zanzibar kutafsiri machapisho yote muhimu ya Kiingereza, vikiwemo vitabu na mashairi kwa Kiswahili ili watu waweze kuyasoma na kuyaelewa.