Kikundi Kazi cha Usimamizi wa Mtandao Tanzania (IGTWG) kimepinga vikali pendekezo la kufungiwa kwa mtandao wa X zamani ukiitwa Twitter.
Chombo hicho kimetoa wito wa kuwepo mbinu ya kusimamia Mtandao ambayo itaheshimu maadili ya kitamaduni na haki za kimsingi.
Wito huo wa kufungiwa kwa "X" nchini Tanzania uliotolewa hivi karibuni, ulipendekezwa kwa mara ya kwanza na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Bw. Mohamed Kawaida, ambaye alidai kuwa mtandao huo unachangia kuzorota kwa maadili kutokana na maudhui ya ngono na kwamba unahimiza ushoga katika jamii ya Watanzania.
Pendekezo hilo liliungwa mkono na makundi tofauti ya kijamii kama vile viongozi wa kidini na kuzua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii.
Hata hivyo, IGTWG inasema katika taarifa yake kwamba pendekezo la kufungiwa kwa mtandao wa 'X' kutokana na kuhimiza ushoga na kuoneshwa kwa maudhui ya ngono lilikuwa hoja dhaifu ambayo haina ushahidi wa kutosha.