Wadhibiti wa Marekani waamuru ukaguzi wa Boeing juu ya suala la mask za oksijeni
2024-07-09 23:00:30| cri

Wadhibiti wa anga wa Marekani wamesema Jumatatu kwamba maelfu ya ndege za Boeing 737 zinahitaji kukaguliwa, huku kukiwa na wasiwasi kwamba mask za oksijeni za abiria zinaweza kushindwa kufanya kazi katika wakati wa dharura.

Maelekezo hayo ya ukaguzi yaliyotolewa na Idara ya Shirikisho la Usafiri wa Anga (FAA) yanaanza kutumika mara moja kwa zaidi ya ndege 2,600 zilizosajiliwa na Marekani. Lengo ni kuhakikisha kuwa majenereta ya kitengo cha huduma za oksijeni kwa abiria yako katika nafasi ifaayo kwenye baadhi ya ndege za Boeing.

FAA ilisema kwenye taarifa yake kwamba makampuni yanapaswa kuangalia majenereta ya oksijeni na kufanya hatua za marekebisho, kama ni lazima, ndani ya siku 120 hadi 150, na kuongeza kuwa maagizo hayo yametokana na ripoti nyingi za majenereta haya kuhama nafasi, na kutaka ufanyike ukaguzi wa jumla wa kuangalia. Ikijibu maagizo hayo, kampuni ya Boeing ilisema kuwa gundi mpya iliyoletwa mwezi Agosti mwaka 2019 baadhi ya wakati ilionekana kuruhusu vitengo vya majenereta ya oksijeni kuhama kwenye nafasi zake.