Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Mpito la Sudan Abdel Fattah Al-Burhan amesisitiza umuhimu wa kufanikisha jukwaa la mazungumzo ya Jeddah.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na baraza hilo, Al-Burhan alitoa kauli hiyo alipokutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Waleed bin Abdulkarim El-Khereiji huko mjini Port Sudan. Majadiliano kati yao yamehusisha wito wa kurejesha jukwaa la mazungumzo la Jeddah. Lakini ameeleza kutoridhishwa na kuwepo kwa chama chochote kinachounga mkono “wanamgambo waasi”.
Tangu mwezi Mei mwaka jana, Saudi Arabia na Marekani zimefadhili mazungumzo kati ya jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yaliyofanyika katika mji wa Jeddah nchini Saudi Arabia ambapo makubaliano kadhaa yalifikiwa lakini baadaye pande hizo mbili zililaumiana kukiuka makubaliano hayo. Mazungumzo ya Jeddah yakasitishwa mwezi Oktoba mwaka jana kutokana na tofauti za kimsingi kati ya pande hizo.