Wasomi wa Ethiopia wamepongeza Pendekezo la Ustaarabu Duniani (GCI) lililotolewa na Rais Xi Jinping wa China na kulitaja kama hatua muhimu kuelekea kujenga mustakbali wa pamoja na kutatua misukusuko ya dunia.
Matamko hayo yalitolewa kwenye mazungumzo ya ngazi ya juu yaitwayo “Mfululizo ya Mihadhara Kuhusu Ustaarabu”, yaliyofanyika Jumamosi mjini Addis Ababa. Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya jumuiya za kiraia za China na Ethiopia.
Kamishna wa jumuiya ya mazungumzo ya kitaifa ya Ethiopia, Yonas Adaye ameliambia shirika la habari la China Xinhua kuwa, GCI limeweka jukwaa kwa mataifa kuwasiliana na kuelewana kuhusu ustaarabu wa upande mwingine kwenye msingi wa ushirikiano wa kunufaishana.
Mshauri mwandamizi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Gedion Gamora amesema, ustaarabu wa China umetoa mfano muhimu kwa nchi za Afrika kutimiza maendeleo ya kasi ya kiuchumi.