Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuzorota kwa hali ya kibinadamu na usalama katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo Jumatatu wiki hii baada ya mawaziri hao kukutana huko Zanzibar, Tanzania, imesema mawaziri hao wamepongeza hali ya sasa ya kusitishwa kwa vita nchini DRC na kupendekeza hali hiyo kudumishwa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mawaziri hao wamejadili hali ya amani, usalama na uhusiano kati ya nchi wanachama, na mchakato wa mafungamano ya EAC. Pia wametambua kuwa mchakato wa kisiasa ni njia inayofaa kufikia amani na usalama endelevu mashariki mwa DRC.