Marais wa China na Guinea-Bissau wafanya mazungumzo mjini Beijing
2024-07-11 08:09:30| CRI

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Guinea-Bissau Umaro Sissoco Embalo wametangaza kuinua uhusiano kati ya nchi zao hadi kufikia ngazi ya Uhusiano wa Wenzi wa Kimkakati, wakati walipofanya mazungumzo jana Jumatano hapa Beijing.

Rais Xi amesema, China inapenda kushirikiana na Guinea-Bissau kukuza urafiki wa jadi, kuimarisha kiwango cha kuaminiana kisiasa, kuendeleza ushirikiano wa kiutendaji, kupanua wigo wa uhusiano wa wenzi wa kimkakati kati ya nchi hizo mbili, na kuisaidia Guinea-Bissau kutimiza maendeleo zaidi.

Rais Embalo amesema Guinea-Bissau itaendelea kusimama kidete na China, kushikilia kanuni ya kuwepo kwa China Moja na kuunga mkono msimamo wa China kuhusu maslahi yake makuu ikiwemo suala la Taiwan. Guinea-Bissau inapongeza maendeleo makubwa yaliyopatikana China na kuichukulia China kama kipaumbele kikuu kwenye mahusiano ya kidiplomasia na mshirika wake muhimu zaidi. Amesema, Guinea-Bissau inatarajia kujifunza uzoefu wa maendeleo ya China, na kuimarisha ushirikiano kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, miundombinu na raslimali za madini.