Mke wa rais wa China Bi. Peng Liyuan, ambaye pia ni balozi wa heshima wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwenye mapambano dhidi ya kifua kikuu na Ukimwi, jana Alhamisi alikutana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi (UNAIDS) Bi. Winnie Byanyima na mkurugenzi mkuu msaidizi wa Shirika la Afya Duniani Bw. Jerome Salomon.
Bi. Peng Liyuan amesema kukomesha Ukimwi na kifua kikuu kuna maana kubwa katika kulinda ustawi wa afya ya binadamu na kuhimiza maendeleo endelevu duniani. Bi. Peng pia amejulisha uzoefu wa China katika kukinga na kudhibiti magonjwa hayo mawili na kueleza kuwa anapendelea kuendelea kutekeleza majukumu ya balozi wa heshima na kutoa mchango zaidi katika mambo hayo.
Bi. Winnie Byanyima na Bw. Jerome Salomon wamepongeza mafanikio iliyopata China katika kupambana na magonjwa hayo na kuendeleza mambo ya afya, na pia wamepongeza mchango uliotolewa na Bi. Peng tangu awe balozi. Wameeleza nia ya kuimarisha ushirikiano na China katika sekta husika, ili kuhimiza maendeleo ya mambo ya afya duniani.