Mashirika yasiyo ya kiserikali yalitangaza Jumapili kwamba raia 23 waliuawa kwa kupigwa risasi na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) katika Jimbo la Kordofan Kaskazini magharibi mwa Sudan,
Shirika lisilo rasmi la Waangalizi wa Haki za Binadamu la Mashad, na Mtandao wa Madaktari wa Sudan, kundi lisilo la kiserikali, yalisema katika taarifa siku ya Jumapili kwamba wanamgambo wa RSF walifanya mauaji katika vijiji kadhaa vya eneo la Al-Rahad na Fangouga katika Jimbo la Kordofan Kaskazini, na kuua raia 23 na kuwajeruhi wengine.
Taarifa ilibainisha kuwa tukio hilo lilitokea wakati kikosi cha RSF kilipokamata magari kadhaa yaliyokuwa yakitoka mji wa Al-Rahad na kuelekea soko la kila wiki la kijiji cha Um Simaima kaskazini mwa mji wa Um Rawaba na kuwafyatulia risasi abiria hao. Hadi sasa RSF bado haijatoa taarifa yoyote kuhusu tukio hilo.
Wakati huohuo jeshi la Sudan (SAF) Jumapili lilisema zaidi ya wapiganaji 100 wa RSF waliuawa na wengine makumi kujeruhiwa katika operesheni iliyofanyika mji mkuu Khartoum siku ya Jumamosi, ambapo idadi kubwa ya magari ya kikosi hicho pia yaliteketezwa.