Idadi kubwa ya wafungwa waliotoroka jela wakamatwa nchini Niger
2024-07-15 08:23:01| CRI

Idadi kubwa ya wafungwa waliotoroka Alhamisi katika gereza lenye ulinzi mkali la Koutoukale, kilomita 50 kaskazini-magharibi mwa mji mkuu Niamey, wamekamatwa na wengine ambao ni magaidi "kupunguzwa kasi" na Jeshi la Ulinzi na Usalama la Niger (FDS).

Likitoa taarifa hiyo Jumamosi jioni jeshi lilisema kutoroka huko kulitokana na uasi uliotokea katika kituo cha rumande, ambapo wafungwa kadhaa walifanikiwa kutoroka.

Lakini kutokana na hatua za "haraka na ufanisi" zilizochukuliwa na vitengo vya usalama vilivyotahadharishwa, idadi kubwa ya waliotoroka walikamatwa, ambapo kwa sasa eneo hilo limezingirwa, na shughuli za utafutaji wa angani zinaendelea ili kuwapata wafungwa waliosalia.

Wakati huo huo, jeshi limesema kitengo chake cha FDS kinachoshika doria katika sekta ya Gorou, katika eneo hilo hilo, kilifanikiwa kuwapata na "kuwavunja kasi" magaidi watatu wenye silaha waliokuwa wakisakwa baada ya kutoroka katika gereza la Koutoukale.

Gereza la Koutoukale liko katika Mkoa wa Tillaberi, eneo kubwa na lisilo na utulivu la mpakani mwa Niger, Mali na Burkina Faso ambalo hukabiliwa na mashambulizi ya waasi wanaohusishwa na kundi la Islamic State na al-Qaida.