Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, watu wanne wameuawa na wengine 42,000 kukimbia makazi yao kufuatia mapigano ya kutumia yaliyotokea hivi karibuni kati ya makabila ya mji wa Luuq, kusini mwa Somalia.
Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Mogadishu, OCHA imesema mapigano hayo ya siku tatu yalianza tarehe 5 mwezi huu katika mkoa wa Gedo na chanzo chake ni tofauti juu ya umiliki wa ardhi.
Ofisi hiyo imesema, watu waliokimbia makazi yao sio tu walikumbwa na mapigano hayo, bali pia katika baadhi ya wakati walilengwa kutokana na makabila yao, na wengine wamekimbia makazi yao kutokana na hofu ya kuathirika moja kwa moja na mapigano hayo.
OCHA imesema, utulivu umerejea katika eneo hilo ingawa bado kuna mvutano mkubwa kati ya pande zinazopingana.