Rais wa zamani Donald Trump, ambaye amekuwa mteule wa chama cha Republican kwa miezi kadhaa Jumatatu alipata kura za kutosha za wajumbe na kuwa mgombea rasmi wa chama hicho.
Rais huyo aliyenusurika katika jaribio la kumwua siku mbili zilizopita, amepata kura nyingi kutoka kwa wajumbe katika Mkutano wa Kitaifa wa Chama cha Republican huko Milwaukee, Wisconsin. Alifikia kiwango cha juu kinachohitajika cha kura kutoka Florida, ambazo zilitangazwa na mwanawe Eric Trump.
Trump ataongoza Chama cha Republican kwenye uchaguzi wa tatu mfululizo, baada ya kumshinda Hillary Clinton mwaka 2016 na kushindwa na Rais wa sasa Joe Biden mwaka 2020.
Trump ametangaza kupitia mtandao wake wa kijamii wa Truth Social kwamba amemchagua Seneta wa Ohio J.D. Vance kama mgombea wake mwenza, na hivyo kumaliza miezi kadhaa ya uvumi kuhusu uteuzi wake wa makamu wa rais.