Sudan Kusini yazindua kampeni ya chanjo ya malaria katika majimbo sita
2024-07-17 08:44:08| CRI

Sudan Kusini Jumanne ilizindua kampeni ya chanjo ya malaria ya R21 katika kaunti 28 za majimbo sita ya nchi hiyo.

Akiongea mjini Juba Waziri wa Afya Yolanda Awel Deng, alisema chanjo hiyo italenga watoto kutoka umri wa miezi 18 hadi miaka mitano katika kaunti 28 za majimbo ya Bahr el Ghazal Kaskazini, Bahr el Ghazal Magharibi, Warrap, Ikweta ya Kati, Jonglei, na Ikweta Mashariki.

Waziri Deng alifafanua kuwa licha ya jitihada zinazoendelea, ugonjwa wa malaria unaendelea kuwa tishio kubwa kwa taifa hilo. Kila mwaka nchi hiyo inakabiliwa na wagonjwa wanaokadiriwa kufikia milioni 2.8 na vifo 6,680, ikimaanisha wagonjwa 7,630 na vifo 18 kila siku.

Uzinduzi wa kampeni ya chanjo hiyo umekuja baada ya serikali kupokea dozi 645,000 za chanjo ya malaria ya R21 Mei 31 kutoka Gavi, Muungano wa Chanjo.

Waziri huyo alibainisha kuwa majimbo yaliyolengwa yalichaguliwa kutokana na kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria, na kuongeza kuwa wizara inalenga kuchanja watoto wapatao 265,897 katika awamu ya kwanza ya chanjo.