Wataalam mbalimbali wameanza mkutano wa siku mbili mjini Nairobi nchini Kenya siku ya Jumanne ili kujadili njia za kuharakisha maendeleo ya jotoardhi barani Afrika.
Baraza la Jotoardhi la Kenya limewaleta pamoja wataalamu, watunga sera, wafadhili, na wawekezaji katika sekta ya jotoardhi kutoka nchi 20 za Afrika ili kuimarisha matumizi ya vyanzo vya nishati mbadala katika bara hili.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati wa Kenya, Alex Wachira, alisema nchi hiyo kwa sasa inazalisha takriban megawati 985 za nishati ya jotoardhi ambapo kuna uwezekano wa kuzalisha hadi megawati 10,000.
Naye meneja wa mradi wa Kituo cha Umoja wa Afrika cha Kukabiliana na Hatari ya Jotoardhi kwa Afrika Mashariki (GRMF), Joseph Mwangi, alibainisha kuwa wakati bara la Afrika linakumbatia magari ya umeme ili kukomesha utoaji wa hewa ukaa katika sekta ya uchukuzi, nishati ya jotoardhi itachukua nafasi muhimu katika kuwezesha mpito huu.
Kwa upande wake mkurugenzi wa mipango na maendeleo katika Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Malawi, Gregory Gamula alisema nchi yake ina nia ya kuongeza uzalishaji wa nishati kwa kutumia rasilimali zake za jotoardhi.