Cote d’Ivoire yatambulisha chanjo ya malaria
2024-07-17 23:12:21| cri

Serikali ya Cote d’Ivoire imetambulisha chanjo ya malaria katika mradi wake wa kuongeza utoaji wa chanjo, ikilenga kuondoa ugonjwa huo itakapofika mwaka 2030.

Katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Robert Mambe, dozi ya kwanza ya chanjo hiyo ilitolewa kwa mtoto wa miezi sita katika eneo maarufu la Abobo mjini Abidjan.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Afya wa nchi hiyo Pierre Dimba amesema, kutambulishwa kwa chanjo ya Malaria kunaashiria hatua kubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao umeendelea kuwa tatizo kubwa kwa jamii, hususan kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Nchini Cote d’Ivoire, ingawa vifo vinavyosababishwa na malaria vimepungua kwa zaidi ya nusu, zaidi ya watoto 1,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanafariki kila mwaka kutokana na ugonjwa huo.