Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) Jumanne lilirekebisha ukuaji wa uchumi wa China wa mwaka 2024 hadi asilimia 5 katika taarifa yake mpya ya Mtazamo wake wa Uchumi wa Dunia (WEO), kutoka makadirio ya mwezi Aprili ambayo yalikuwa asilimia 4.6.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo marekebisho hayo kimsingi yanahusishwa na kuongezeka kwa matumizi ya kibinafsi na mauzo makubwa ya nje katika robo ya kwanza. IMF ilidumisha makadirio yake ya ukuaji wa kimataifa mwaka 2024 ya asilimia 3.2, ikibainisha kuwa uchumi unaoibukia wa Asia unasalia kuwa chachu kubwa ya uchumi wa dunia.
Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas alisema katika blogu kwamba ukuaji wa uchumi katika nchi za India na China unarekebishwa kwenda juu na kuchangia karibu nusu ya ukuaji wa kimataifa.
Marekebisho ya makadirio ya ukuaji wa China yalitangazwa mwishoni mwa mwezi Mei na naibu mkurugenzi mkuu wa kwanza wa IMF, Gita Gopinath, wakati wa mkutano na wanahabari mjini Beijing kufuatia kumalizika kwa Mashauriano ya mwaka 2024 ya Kifungu cha IV cha timu ya IMF kwa China.