Ofisi ya chombo cha habari cha kundi la Hamas ilitoa taarifa ikisema, mashambulizi mawili yaliyofanywa na jeshi la Israel Jumanne katika Ukanda wa Gaza yamesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 40.
Taarifa hiyo ilisema shambulizi lililotokea katika shule ya Al-Razi inayohusiana na Umoja wa Mataifa iliyoko kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, katikati mwa Gaza limesababisha vifo vya Wapalestina 23, na wengine 73 kujeruhiwa.
Ofisi hiyo ilisema shambulizi lingine lililotokea eneo la al-Mawasi huko Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza limesababisha vifo vya Wapelestina 17, na wengine 26 kujeruhiwa.
Kikosi cha Ulinzi cha Israel (IDF) kilisema katika taarifa siku ya Jumanne kwamba kulingana na taarifa za kijasusi, Jeshi la Anga la Israel (IAF) liliwashambulia "magaidi" waliokuwa wakiendesha shughuli zao katika shule ya UNRWA katika eneo la Nuseirat.