Shirika la ndege la Uganda latangaza kuzindua safari 3 mpya barani Afrika
2024-07-18 08:56:49| CRI

Shirika la ndege la Uganda limetangaza kuzindua safari tatu mpya zitakazoelekea miji mikuu ya Zambia, Zimbabwe na Nigeria mwezi Septemba mwaka huu wa 2024.

Katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika Jumatano mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda, afisa mkuu mtendaji wa Shirika la Ndege la Uganda, Jenifer Bamuturaki amesema kuwa safari hizo mpya zitaiunganisha zaidi Uganda na maeneo mengine ya Afrika. Kuzinduliwa kwa safari mpya ni hatua muhimu katika kutoa mchango endelevu kwa safari za ndani ya Afrika. Pia safari hizi za Magharibi na Kusini mwa Afrika zitaleta urahisi kwa wasafiri katika bara zima, na kuleta fursa nyingi katika biashara, utalii, na uhusiano wa kijamii na kitamaduni.

Shirika hilo tayari linasafiri katika nchi za Kenya, Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Somalia, Sudan Kusini, Afrika Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu, India, Burundi na mji wa Lagos wa Nigeria.