Waangalizi wa kimataifa waipongeza Rwanda kwa mchakato wa uchaguzi wa amani na makini
2024-07-18 08:59:29| CRI

Waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi Jumatano waliipongeza Rwanda kwa kudumisha "mazingira ya amani ya uchaguzi" na usimamizi wa makini wakati wa uchaguzi mkuu uliomalizika hivi majuzi.

Katika taarifa ya pamoja iliyosomwa wakati wa mkutano na wanahabari mjini Kigali nchini Rwanda, waangalizi hao wanaowakilisha mashirika kama vile Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Umoja wa Afrika (AU), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati, walipongeza mchakato mzima wa uchaguzi.

Taarifa hiyo ilisema pia walitambua kazi ya bidii ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Rwanda (NEC) na taasisi nyingine zinazohusika kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi, kwamba uchaguzi ulifanyika katika hali ya utulivu na amani iliyowawezesha wagombea kufanya kampeni kwa uhuru.