Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeikabidhi Serikali ya Tanzania dozi milioni 3.9 za chanjo ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo kwenye hafla iliyofanyika jumanne wiki hii jijini Arusha wakati wa ufunguzi wa warsha ya ushirikiano wa serikali na sekta binafsi kwenye eneo la afya ya wanyama.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa chanjo hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania Prof. Riziki Shemdoe amelishukuru Shirika hilo kwa msaada huo, na kusema hatua hiyo inaunga mkono mipango ya Serikali kupitia Wizara yake kwa mwaka huu wa fedha ambapo imetenga takribani Sh bilioni 28 kwa ajili ya kuendesha zoezi la chanjo ya mifugo nchi nzima.
Kwa upande wake Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania, Stela Kiambi, amesema Shirika hilo linatambua kuwa afya bora ya wanyama inachangia afya bora ya binadamu hivyo litaendelea kushirikiana na Wizara husika kwenye kampeni yake ya kutoa chanjo ya wanyama nchini kote inayotarajia kuanza wakati wowote.